MKUU wa wilaya ya Lushoto mkoani
Tanga, Alhaj Majid Mwanga amempa muda wa mwezi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Lushoto Jumanne Shauri kuhakikisha zahanati ya Migambo inapatiwa huduma
umeme ndani ya kipindi hicho ili iweze kuwahudumia wagonjwa wakati wote.
Agizo hilo la DC Mwanga limetokana
na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kupitia
mikutano ya hadhara kwenye kijiji cha Migambo ambapo alibaini changamoto kubwa
iliyokuwa ikilalamikiwa dhidi ya zahanati hiyo kukosa ni kukosekana kwa nishati hiyo muhimu.
Amesema kimsingi nishati hiyo ni
muhimu sana hasa kwenye maeneo ya utoaji huduma hivyo kuamua kutoa agizo hilo
ili kuiwezesha zanahati hiyo kufanya kazi zake wakati wote kitendo ambacho
kitasaidia kupunguza vifo ambavyo vinaweza kutokana na kukosekana kwa huduma
nyakati za usiku.
Amesema ameshangaa kuona zanahati
hiyo ikiwa haina nishati wakati nguzo za umeme zimepita karibu na eneo hilo
hivyo kutaka suala hilo lishughuliwe ipasavyo lengo likiwa kupatikana ufumbuzi
wa changamoto hiyo.
kufuatia hali hiyo,mkuu huyo wa wilaya amewaagiza wakurugenzi
wote wa halmashauri mbili zilizopo wilayani humo kuhakikisha mikutano yote ya
vijiji inafanyika kwa mujibu wa sheria zilizopo ikiwemo kusomwa kwa mapato na
matumizi kwa watendaji wa maeneo husika lengo likiwa kurudisha mrejesho kwa
wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo yaliyofanyika.


0 comments:
Post a Comment