photo tyyyyyyyyyyyyyyyy_zpsd20272cf.jpg

WAKONGWE WANAAMINI NYERERE BADO ANAISHI.

Miaka 15 imetimia leo tangu nchi yetu iondokewe na kiongozi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa msiba wake haujawahi kuisha, bali umebakia kuwa wa kipekee katika nchi yetu. Msiba huo una simulizi lukuki na haufutiki. Kwa kifupi, nchi yetu haijapata kiongozi wa aina au mfano wake, ambaye tunaweza kusimama na kujiridhisha kuwa ni kama yeye.
Kwa wale waliobahatika kumwona, kuishi na hata kufanya kazi naye, wanaamini bado anaishi na atandelea kuishi. 

Ndiyo maana wakati akitangaza kifo chake siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alilieleza Taifa kwamba kifo chake kilikuwa pigo kubwa, si tu kwa Tanzania, bali pia kwa ulimwengu mzima kutokana na kuwa nguzo imara na mtetezi wa utu na haki za binadamu. 

Hivyo, tunapojaribu kufanya kumbukumbu ya miaka 15 bila kuwa naye, ni muhimu kwetu kama Taifa kujitafakari upya, tena kwa kina ili tuone ni jinsi gani tunaendelea kuyaishi mazuri yote aliyotuachia au yale aliyoyafanya.
Ni vyema kutambua kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa mwanadamu, hakuwa mkamilifu. Bila shaka alikuwa na kasoro na upungufu hapa na pale, ambao hatuna budi kuutumia kama changamoto katika nafsi zetu ili tuweze kusonga mbele. 

Tuitumie kumbukumbu yake inayofanyika nchini kote leo kwa njia mbalimbali, ikiwamo ibada, kongamano, warsha na mijadala ya kisiasa kujiuliza swali hili: Sisi tuliobaki hapa duniani tunafanya nini ili kujaribu kuyaishi mazuri yote aliyoyahubiri na kuyasimamia? Pia ipo mifano mingi ya mambo aliyoyakataa na kuyapinga kwa dhamira safi kabisa.
Tunamkumbuka jinsi alivyopigania usawa wa binadamu. Kamwe hatuwezi kusahau alivyopigana dhidi ya ubaguzi wa rangi, alivyopinga unyanyasaji, unyonyaji na uonevu mwingine, ambao bado umeota mizizi duniani kote. 

Kauli yake ilipokewa kila kona ya dunia kama sauti ya kutetea wanyonge. 

Hapa nchini alikuwa mwadilifu wa kutolea mfano, huku akihakikisha mali na rasilimali za nchi zinalindwa na kutumiwa kwa usawa na bila ubaguzi. 

Alijitahidi kusimamia maadili ya Taifa yaliyobainishwa katika Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Ni jambo la kusikitisha kwamba mambo mengi mema aliyotuachia tumeyapiga teke, badala yake tumekumbatia na kuiga yale yasiyofaa. 

Hivi sasa nchi yetu imekosa dira na mwelekeo. Miaka 15 baada ya kifo chake, hata baadhi ya wasaidizi na wafuasi wake ambao walitegemewa kuyaenzi na kuyaendeleza maono na mafundisho yake, wamebadilisha mwelekeo. 

Tumeshuhudia upinzani mkubwa ndani ya lililokuwa Bunge la Katiba, wajumbe wengi wamekataa tunu za Taifa kama uadilifu na maadili ya uongozi zisiingizwe katika ‘Katiba Inayopendekezwa’.
Kwa hiyo, Mwalimu tunayejaribu kumkumbuka leo kwa shughuli kama ya kuzima Mwenge wa Uhuru aliouanzisha, akisema utawamulika maadui ndani na nje ya mipaka ya nchi, hatumthamini tena kwa vitendo. 

Maadhimisho kama ya leo yamebaki kufanyika kwa mazoea tu, kwani yamepoteza maana na uhalisia. 

Nini kimesababisha hali hiyo ni swali linaloweza kujibiwa tu na viongozi wetu. Mwalimu angeibuka leo, angalau kwa dakika moja, akaiona nchi aliyoiacha, bila shaka angeshtuka, kwani tumebaki kuwa nchi iliyogawanyika. 

Angeshtuka kuona wale wanaopaswa kutuleta pamoja ndio walewale wanaotugawa katika mafungu kwa kuendekeza siasa za chuki, badala ya kuhubiri umoja na mshikamano alioturithisha kama Taifa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment