![]() |
| CHADEMA, NCCR MAGEUZI, CUF NA NLD WAUNGANA LENGO KIKISAMBASATISHA CHAMA CHA MAPINDUZI"CCM"MADARAKANI 2015.... |
VYAMA vinne vya upinzani nchini
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), jana vilitiliana saini
ya makubaliano ya ushirikiano, ikiwamo kusimamisha mgombea katika
chaguzi zote, kuanzia wa serikali za mitaa mwaka huu na ule wa wabunge,
madiwani na rais mwaka kesho.
Vyama hivyo ni Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National
League for Democracy (NLD).
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa
alisoma makubaliano hayo kwa niaba ya makatibu wakuu wa vyama hivyo.
Alisema ushirikiano huo watauanza kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,
utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Alisema kupitia makubaliano hayo, vyama
vyote vinne vimekubaliana kuhuisha sera zao na kuchukua yale
yanayofanana na kila chama kuyazungumzia hayo kwa wananchi.
"Utaratibu wa namna gani vyama vyetu
vitashirikiana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji
mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 utatolewa katika wakati
mwafaka kwa ngazi zote ili waweze kuutumia kama mwongozo wa kufanya
kazi,” alisema.
Alisema pia watashirikiana katika
mchakato wa kuelimisha umma. kuifahamu na kuipigia kura ya hapana Katiba
Inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba, ambayo alisema
haijazingatia maslahi,wala maoni ya wananchi.
Alisema vyama hivyo pia vitajenga
ushirikiano wa dhati katika mambo yote na hoja zote za kitaifa na zenye
maslahi kwa Watanzania.
Aidha, umoja huo uliahidi kulinda
Muungano bila kuwa na migongano ya maslahi, kama inavyojidhihirisha
katika Katiba Inayopendekezwa.
Slaa alisema pia watahimiza na kusimamia
ushirikiano wa pamoja baina ya vyama, asasi na makundi ya Watanzania
wenye njia ya dhati ya kulinda na kuenzi muungano bila kunyenyekea
maslahi binafsi ya makundi, kabila na itikadi.
Naye, Katibu Mkuu wa CUF na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alisema
Wazanzibar hawaungi mkono katiba hiyo huku Mwenyekiti wake, Profesa
Ibrahim Lipumba akisema katiba hiyo imelenga kuwalinda baadhi ya
mafisadi ndani ya CCM.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James
Mbatia alisema makubalinao ya vyama hivyo ni kwa maslahi ya taifa na si
vyama vyao. Alisema anashangaa kauli za utata zinazotolewa, hivyo
kufanya viongozi hao kutoaminika kwa jamii.
Mwenyikiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alimpongeza Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi. Pia Mbowe alisema
kiongozi au mwanachama yeyote wa Chadema, ambaye atakuwa na lengo la
kufifisha juhudi za UKAWA ni vyema akajiondoa, kwa kuwa hawatamvumilia.
Mshikamano baina ya viongozi wa vyama
hivyo ulianzia katika Bunge Maalumu la Katiba baada ya kususia vikao,
wakidai wanapuuzwa na wenzao wa CCM ambao kimsingi ni wengi katika bunge
hilo.
Hata hivyo, wingi wa CCM haukutokana na upendeleo, bali kwa nafasi walizonazo kama wawakilishi wa wananchi.
Wapinzani hao kwa kuungana kwao,
wanaamini watakuwa na uwezo wa kukisambaratisha chama tawala cha CCM, katika uchaguzi wa serikali za mitaa, udiwani,ubunge na hata katika nafasi ya Urais
hapo mwakani 2014.



0 comments:
Post a Comment