WAKATI joto la Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa mwaka
kesho likizidi kupanda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
amewashangaa wanaojitokeza kutangaza nia ya kuwania Urais, akisema
nafasi hiyo ni nyeti ambayo wengi wanapaswa kuogopa kutangaza kuitaka.
Badala yake, ameshauri wasubiri wafuatwe na watu wenye `kuona mbali’ kwa lengo la kuwashawishi kuwania nafasi hiyo.
“Hapo zamani kuna kikao kilikaa watu wakasema na tumuumbe mtu kwa
sura na mfano wetu. Na baadaye kikao kikakaa tena wajumbe wakasema
tumtume nani…ndivyo inavyopaswa kuwa kwa nafasi ya Rais wa nchi pia,”
alisema Nyalandu akiwa mjini hapa.
Alisisitiza kuwa, nafasi ya urais ni kubwa sana hivyo yeye binafsi
hawezi kujitangazia nia ya kuwania nafasi hiyo na kuwabeza wachache
wanaojitangaza akisema wanafanya makosa.
Alisema kwa uzito wa nafasi ya urais mtu hawezi kuibuka na
kujitangazia kuitaka nafasi hiyo, bali anapaswa asubiri kushawishiwa na
watu wengine watakaomwona anafaa kuwaongoza na kuwaletea maendeleo.
Nyalandu hakuweka wazi iwapo atagombea au hatogombea, lakini
aliendelea kusisitiza kuwa watu wanapaswa kusema na si mtu binafsi
kujisemea.
Aliwataka Watanzania kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze
kuwachagulia Rais atakayekuwa msikivu, mwelewa na mwenye kutambua
umuhimu wa kuwajali watu anaowaongoza.
Wakati Nyalandu akiyasema hayo, watu kadhaa kutoka ndani ya chama
tawala, CCM wameshaelezea nia yao ya kutaka kuwania urais mwaka kesho,
akiwemo Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla.
Wengine wanaotajwatajwa kwa nafasi hiyo na hata kujikuta wakiingia
matatani na chama chao kilichowaita na kuwaonya kutojiingiza katika
harakati zozote za kuwania nafasi ya chama hicho hadi muda mwafaka
utakapofika ni mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward
Lowassa.
Wamo pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari
Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Sera na Uratibu, Stephen Wasira.
Akizungumzia tuhuma ambazo amekuwa akitupiwa kupitia gazeti moja la
hapa nchini, Nyalandu aliendelea kusisitiza kuwa gazeti hilo linatumiwa
na wahusika wa ujangili ili liweze kumchafua na kuondolewa katika nafasi
hiyo.
Alisema anaamini utendaji kazi wake mzuri ndiyo sababu hasa ya gazeti
hilo kutumika kumchafua kwakuwa anaonekana kuziba mianya ya ujangili
waliyokuwa wakiitumia kabla ya yeye kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili
na Utalii.
Nyalandu alisisitiza kuwa hatorudi nyuma katika kupigana vita ya
ujangili hususani wa kuua tembo na badala yake atazidi kuweka mikakati
yenye kulenga kulinda maslahi ya Taifa.



0 comments:
Post a Comment