![]() |
| BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limelaani vikali kukithiri kwa muendelezo wa matukio ya ukiukwaji sheria |
BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limelaani
vikali kukithiri kwa muendelezo wa matukio ya ukiukwaji sheria na haki za
binadamu unaofanywa na jeshi la polisi na serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Kauli hiyo, imetolewa jana na Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Patrobass
Katambi, wakati akitoa tamko kwa niaba ya Vijana na wadau wa amani, haki na
usawa duniani kote.
Alisema CCM inatumia jeshi la Polisi kutekeleza malengo yake ya kisiasa ili
kuua ushindani wa kisera.
Alisema kwa mjibu wa ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, inayosema kila binadamu wamezaliwa huru na wanayo haki sawa na
wanapaswa kuheshimiwa, pia ibara ya 13 (3) inatoa ulinzi wa haki za kiraia,
kimajukumu na matakwa ya mtu au jamii na 13 (4) inaagiza mtu yeyote
kutobaguliwa na mtu au mamlaka yoyote.
“Tunaitaka Serikali itoe tamko na iwatangazie Watanzania na Umoja wa Mataifa
kama ibara ya 3 (1),12, 13, 14, 18 na 21 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
Mwaka 1977 hazitumiki na Serikali haizitambui mbali na viapo vya kuitii na
kuilinda kwa viongozi wote akiwemo Rais Jakaya Kikwete.
“Pia serikali iwatamkie kwamba utii wa sheria bila shuruti utekelezwe na
raia, vyama vya upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu na wanahabari na
siyo viongozi wa serikali, polisi na watawala,” alisema Katambi.
Aidha, alisema Serikali ya Tanzania itangaze kuwa haitambui na haifungwi na
tamko la ulimwengu la haki za binadamu mwaka 1948 ya mkataba wa kimataifa
unaopinga unyanyasaji na kutesa binadamu na mkataba wa haki za kisiasa na za
kiraia 1966, pia na mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na watu.
Alisema, Sheria ya vyama vya siasa ya Mwaka 1992 na Katiba ya Tanzania ya
1977, zinatoa haki ya maandamano ya amani kupinga ukiukwaji wowote wa haki,
usawa, sheria, taratibu au kanuni msingi ya asili na kama inazitambua,
iwachukulie hatua watendaji waliokiuka matakwa ya sheria.
Katika hatua hiyo, alisema endapo Serikali itapuuza malalamiko na madai
dhidi ya unyama huo unaofanywa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na chama
tawala, hawatasita kuingia mtaani kupambana na kujichukulia sheria mkononi.



0 comments:
Post a Comment