MWENYEKITI wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (BAVICHA), Mkoa wa Iringa Joseph Lyata, amemlipua Mbunge wa
Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe kuwa ni mbabaishaji na kuwataka wananchi
wa Kyela kumng’oa katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema Dk. Mwakyembe ni kigeugeu, kwani yuko tayari kuyakana hata
mawazo yake na kutolea mfano kuwa, mbunge huyo ni muumini wa Serikali
tatu, lakini ulipofika wakati wa kujadili rasimu ya Katiba, aliyakana
mawazo yake jambo ambalo ni hatari kwa kiongozi wa aina hiyo, kwani ipo
siku anaweza kuwauza wananchi wake.
Aliongeza kuwa, mbali na kujipambanua kuwa ni mpiganaji wa vita dhidi
ya ufisadi ni vigumu kwa kiongozi huyo kufanikiwa, kwani asilimia kubwa
ya watu wanaofanya ufisadi katika wizara yake ndiyo wafadhili wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Lyata, alisema Dk. Mwakyembe kamwe haiwezi Wizara ya Uchukukuzi,
kwani vitengo vyote vimeshikiliwa na wakubwa ambao sehemu kubwa ndiyo
wafadhili wa CCM inayounda Serikali anayoiongoza.
“Dk. Mwakyembe alikuja na kasi ya ajabu, alianza na viwanja vya
ndege, ameona kwa moto, akageukia Bandari nako kuchungu, alipojaribu
kugeukia reli kumbe kule nako ni hatari, hivyo ni vigumu kwa waziri huyo
kufanikiwa.
Dawa ni kumuondoa katika uchaguzi ujao,” alisema Lyata.
Alisema sifa anayopewa Dk. Mwakyembe, haifanani na haiba aliyonayo,
kwani amekuwa akipewa sifa kama kiongozi mpiganaji wakati ni kigeugeu.
Alisema Wilaya hiyo ina miundombinu mibovu wakati Waziri Mwakyembe
anahusika na barabara, lakini ameshindwa kuboresha za jimboni kwake.
Katika hatua nyingine, viongozi hao wa BAVICHA walisema
wanasikitishwa na hatua ya baadhi ya wananchi kutembea vifua mbele kuwa
wao ni CCM damu, ili hali viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho ndio
wanaofaidi.
Naye Makumu Mwenyekiti BAVICHA Taifa, Patrick Ole Sosopi, alisema
kuwa licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi, bado ni masikini
kutokana na viongozi wengi waliopewa dhamana ya uongozi kuwa wabinafsi.
Makumu huyo, alisema kutokana na viongozi wengi kuwa wabinafsi na
muda wote wanawaza uchaguzi, wanakosa nafasi ya kuwatumikia wananchi na
kwamba Tanzania inashindwa kupiga hatua kutokana na watu waliopewa
dhamani kutokuwa na uchungu na taifa hili.
“Ndugu zangu Wanaipinda na Kyela kwa ujumla, nchi hii haipigi hatua
kimaendeleo kwani watu tuliowapa dhamana si viongozi bali ni madalali
ambao wanawaza familia zao tu na ili kuondoka na watu hawa niwaombe
likianza zoezi la uandikishaji katika daftari kudumu, mjitokeze kwa
wingi ili mshiriki vyema uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa maana ya
wenyeviti wa vitongoji,vijiji na mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Aidha katika hatua nyingine, Sosopi alisema viongozi wa CCM chini ya
aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta wameingia
katika historia ya ajabu kwa kuruhusu marehemu kupiga kura kupitisha
Katiba inayopendekezwa.
“Samwel Sitta na wenzake wanajitapa kwamba Katiba hii ni ya
kihistoria. Hii ni sahihi kwani hakuna popote duniani isipo kuwa
Tanzania tu ambapo hata marehemu wanapiga kura kupitisha Katiba wakati
wa kutafuta theruthi mbili ili kuungwa mkono,” aliongeza Sosopi.
Aliwataka wananchi hao kuiadabisha CCM wakati wa kura za maoni kupitisha Katiba, inayotarajiwa kufanyika Aprili mwakani.



0 comments:
Post a Comment