![]() |
Polisi wachana bango la walimu linalohoji posho Bunge Maalumu |
Maandamano ya walimu kuingia katika
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani, jana
yalipata mtafaruku baada ya polisi kuyaingilia na kuchana bango mojawapo
lililohoji posho za wajumbe wa Bunge la Katiba.
Bango hilo la kitambaa cheupe lilikuwa na
maandishi yanayohoji posho ya Sh300,000 waliyokuwa wanapata wajumbe wa
Bunge la Katiba, yakilinganishwa na kazi kubwa wanayofanya walimu.
Ujumbe wenyewe ulisomeka hivi: “Haki iko wapi
usawa uko wapi, posho ya mjumbe wa Bunge la Katiba kwa siku shilingi
laki tatu, mshahara wa mwalimu shilingi 370 kwa mwezi. No big results
without big salary (Hakuna matokeo makubwa bila mshahara mkubwa)”.
Ujumbe huo ulikuwa ukifanya rejea ya viwango vya
malipo ya Sh300,000 kwa siku ambazo walikuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge
Maalumu zikiwa ni Sh230,000 kama posho ya kujikimu na Sh70,000 ambazo ni
posho ya vikao.
Hata hivyo bango hilo lilichanwa hatua chache
kabla ya walimu hao hawajaingia uwanjani humo, ambapo mgeni rasmi
alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
mkoani Kagera Dauda Bilikesi, alisema amesikia habari za bango hilo
kuharibiwa lakini akasema asingezungumza kwa kina kuhusu suala hilo kwa
kuwa hayo yamepita.
MASHAIRI NAYO YATUMIKA
Muda mfupi baada ya polisi kuharibu bango hilo
lisionekane uwanjani, walimu hao walipiga chenga kiana wakaibuka na
ujumbe ule ule kwa njia ya shairi.
Kupitia shairi hilo liliposomwa mbele ya Pinda,
walimu walihoji ukubwa wa posho za wajumbe wa Bunge la Katiba
zikilinganishwa na mshahara wanaopata, hali iliyosababisha umati wa
walimu uliokuwa uwanjani hapo kulipuka kwa sauti kubwa za shangwe.
Shairi hilo lililosomwa na Mwalimu Betwel Magoso
kutoka Wilaya ya Biharamulo, lilisababisha kuvurugika kwa muda kwa
utaratibu uliopangwa kwa mujibu wa ratiba, pale alipohoji wajumbe wa
Bunge la Katiba kupata Sh1 milioni kwa siku tatu ambazo ni mkopo wa
mwalimu kwa miaka mitatu.
Mwalimu Magoso alimgusa Pinda ambaye kabla ya
kuanza hotuba yake alianza kwa kusema kuwa mwalimu huyo alitumia ujanja
kufikisha ujumbe wake na kuwa baadhi ya maneno katika shairi lake
yalikuwa ni mazito.



0 comments:
Post a Comment