MIRADI ya ujenzi katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, imeghubikwa
na tuhuma za ufisadi, ambapo hivi karibuni imekabidhiwa nyumba ya
mwalimu yenye vyumba viwili vya kulala na sebule, ikitajwa kugharimu sh.
milioni 89, jamba ambalo limeibua utata na kumlazimu Mkuu wa wilaya
hiyo, Elibariki Kingu kuingilia kati.
Gharama ya ujenzi wa nyumba hiyo katika shule ya sekondari Ichama
kata ya Chabutwa ni sehemu ya matumizi ya kiasi cha sh. milioni 219
zilizotolewa na Serikali kuu kupitia mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Sekondari (MMES) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa mbali na kiasi
hicho pia katika muendelezo wa matumizi ya fedha hizo, sh. milioni 8.6,
zimetumiwa kwa ajili ya kujenga tanki la kuvunia maji ya mvua katika
nyumba hiyo, hali inaibua maswali kwa wakazi wa Chabutwa kutokana na
ubora wa nyumba yenyewe na gharama zinazotajwa kutumika.
Kutokana na utata huo, tayari mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki
Kingu, ameingilia kati na kutaka malipo ya mradi huo yasitishwe huku
akiagiza wataalam wa halmashauri kufanya tathmini upya kuthibitisha kama
thamani ya fedha inalingana na ubora wa nyumba.
Oktoba 8 mwaka huu, wakati kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru
kitaifa, Rache Kasanda akiikagua nyumba hiyo ya mwalimu baada ya
kuifunga, alisikika akisifia kuwa ni bora kwa kile alichoeleza kuwa
haina dalili yoyote ya nyufa.
Gazeti hili lilipomhoji juu ya gharama zilizotajwa katika taarifa ya
halmashauri kama zinarandana na ubora wa nyumba, Kasanda alisema
wahusika walimueleza kuwa gharama zilizoandikwa katika taarifa zilikuwa
zimekosewa na kwamba nyumba imegharimu sh. milioni 38 na si 89 iliyosoma
kwake.
“Wasaidizi wangu ulioongea nao awali waliniambia juu ya hilo na
nikafuatilia na mkurugenzi ameniambia walikosea katika kuandika na
kwamba gharama zake ni sh. milioni 38,” alisema Kasanda akiwa katika
kata ya Simbo.
Nyumba hiyo ina vyumba viwili vya kulala visivyokuwa na vyoo vya
ndani, sebule moja pamoja na madirisha manne yaliyowekwa nondo na nyavu,
huku sakafu yake ikiwa ya kawaida ya saruji na kuezekwa kwa bati.
Kwa mujibu wa taarifa fupi ya ujenzi iliyosomwa kwa kiongozi wa mbio
za mwenge, mbali na sh milioni 89 gharama za nyumba hiyo, pia zimetumika
sh .milioni 58.5 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha maabara, sh. milioni
38.8 kwa ajili ya vyumba viwili vya madarasa na sh. milioni 23.9 kwa
ununuzi wa samani.
Mmoja wa maofisa wa Kampuni ya ukandarasi ya Elisha & Son Ltd ya
mjini Igunga, iliyopewa kazi ya ujenzi wa majengo hayo, alipoulizwa
gharama za nyumba ya mwalimu alisema hazizidi sh. milioni 50 na si chini
ya milioni 40.
“Kama wanasema ni sh. milioni 89 sasa unanifumbua macho labda kuna
mkataba unaotuhusu sisi na ule unaohusu taarifa zao mbele ya umma lakini
hizo gharama za nyumba hazifiki huko,” alisema.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Igunga, Rustruka Turuka alipoulizwa
gharama halisi ya jengo hilo, alielekeza swali hilo kwa Afisa Elimu
Sekondari, Aloyce Kaziyareli ambaye alisema gharama zilizosomwa siku ya
uzinduzi ndizo zinapaswa kufuatwa.
“Gharama ni hizo hata hiyo nyumba ndiyo gharama yake, sasa ukitaka
kujua zimefikaje hayo ni maswali ya Mkandarasi,” alisema Kaziyareli.
Jana, mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, alizungumza na
gazeti hili na kukiri kuwaita badhi ya maofisa wa halmashauri katika
ofisi yake kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa ubora wa mradi huo na fedha
zilizotumika.
Alisema baada ya kuongea nao aliwaagiza kusitisha malipo kwa
mkandarasi na kisha mthamini wa ujenzi wa halmashauri awasilishe taarifa
yake ya kukubali jengo hilo la walimu kuwa na thamani ya sh. milioni
89.
Kwa mujibu wa Kingu, baada ya hatua hiyo wataalam mbali mbali
wataenda kufanya tathmini upya kuthibitisha kama nyumba iliyojengwa ina
thamani ya fedha iliyotajwa.
Huyu aliyepitisha BOQ ya fedha hizo tunamtaka ajieleze kwa kuwa jengo
halilingani na thamani ya fedha iliyotajwa,” alisema Kingu.



0 comments:
Post a Comment