WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imepigilia
msumari kwa kuendelea kuwazuia wanafunzi wa shule za sekondari za serikali za
bweni na kutwa kumiliki simu za mkononi wakiwa shuleni na yule atakayekamatwa
hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Licha ya kuendelea kukazia amri hiyo, pia imetoa
utaratibu unaowataka wakuu wa shule za sekondari za mabweni kuzitumia ofisi za
walimu wa malezi kuwa ni sehemu muafaka ya kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo
mbalimbali ya kuwasiliana na wazazi na walezi wao.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, jana, wakati alipojibu maswali ya
wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe, ambayo ni ya wavulana wa vipaji
maalumu, ambao baadhi yao walimwomba Waziri aruhusu matumizi ya simu za mkononi
kwa wanafunzi wa shule za sekondari wakiwa shuleni.
Akijibu swali la msingi la Mwanafunzi Hamis
George wa kidato cha sita mchepuo wa PCB, ambaye alisema kuwa hakuna mantiki
yoyote kwa wakati huu Serikali kuendelea kupiga marufuku kwa wanafunzi wa
sekondari za serikali wa bweni kuwa na simu za mkononi kwani zitawasaidia
kuwasiliana na wazazi, walezi nyakati za shida shuleni.
Hoja hiyo ilipingwa na Waziri Kawambwa akisema
kuwa maudhui ya uzuia simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule za sekondari za
Serikali bado halijabadilika na litaendelea kuwepo kutokana na hali halisi ya
kimazingira yaliyopo.
“ Hili suala nikiwa Waziri mwenye dhamana ,
siwezi kulitengua, litaendelea kusimama kama ilivyo, maelekezo ni kwamba wakuu
wa shule waandae utaratibu wa kuzitumia ofisi za walimu wa malezi kuwa ni
sehemu ya wanafunzi kupeleka matatizo yao yapatiwe ufumbuzi na si kuruhusu
mwanafunzi kuwa na simu shuleni,” alisema Waziri huyo.
Hoja hiyo ya kuendelea kupinga marufuku wanafunzi
wa shule za sekondari kuwa na simu shuleni, iliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya
Mvomero, Anthony Mtaka, ambaye aliwakata wanafunzi kufuata kile kilichowaleta
shuleni, kwani miaka minne ama miwili kwao si mingi wakimaliza wataenda
kukumbana na maisha ya kidunia mtaani.
“ Mwanafunzi upo hapa Mzumbe Sekondari kwa ajili
ya kusoma...kuwa na simu haikusaidii , kwanza utajipotezea muda kwa kuchati na
watu ama marafiki wa kike , mwishowe unafeli mtihani, lawama zitaelekezwa
serikalini…vuteni subira mambo haya yanawasubiri baada ya kumaliza elimu yetu
ya sekondari,” alisema Mkuu wa Wilaya.



0 comments:
Post a Comment