NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba amesema hakuna mwanasiasa yeyote anayemhofia kuwa
kikwazo katika harakati zake za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania baada ya kutangaza nia hiyo Aprili mwaka huu. Januari alitangaza nia
hiyo alipokuwa akihojiwa katika kituo cha Dira ya Dunia kinachorushwa na kituo
cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Katika mahojiano maalumu aliyofanya jana na wawakilishi
wa vyombo mbalimbali vya habari wa mjini Iringa waliotaka ufafanuzi kuhusu nia
yake hiyo Makamba alisema;
“Huu ni msukumo wangu unaotokana na dhamira yangu
ya dhati ya kuleta aina mpya ya uongozi utakaosaidia kuipeleka nchi mbele zaidi
na nimejipanga kushinda.”
Alikutana na wanahabari hao ikiwa ni siku moja
baada ya kushiriki mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Mtera inayomilikiwa na
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa.
Kutumiwa na Lowassa January alitumia fursa hiyo
pia kukanusha uvumi wa baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wanaodai kwamba
anatumiwa kisiasa na Waziri Mkuu wa zamani ambaye kwa sasa ni Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa anayetajwa pia kuwania nafasi hiyo.
“Mimi ni mtu mzima, nina utashi wangu, nina familia
yangu, nina mke na watoto, nina jimbo, nina nyadhifa serikalini na kwenye
chama, kuniambia mimi nafanya jambo fulani kwa sababu ya mtu fulani ni matusi
makubwa sana,” alisema.
Alisema watu wanaosema hayo wanakosea sana na kwa
bahati mbaya watu hao hawamjui alivyo na kwamba wanapaswa kumuomba radhi.
January ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM alisema;
“huo unaweza kuwa mkakati na mbinu chafu za
kumpunguzia mtu mwingine nguvu za kisiasa ili watu wanaokuamini wakate tamaa,
hata hivyo huko mbele mambo haya yatajulikana.”
Pamoja na kukanusha kuwa nyuma ya mtu yeyote
katika harakati zake hizo, alisema wapo wengine wanaozihusisha harakati zake za
sasa na uchaguzi wa miaka mingine ijayo jambo ambalo pia alisema si la kweli.
“Ukiingia kugombea nafasi za uongozi halafu
hufanyi kwa dhamira ya dhati ya sasa wewe hufai kabisa kuwa kiongozi; hayo
mawili nayasikia na naomba Watanzania wajue kwamba si ya kweli,” alisema.
Uzoefu wa kisiasa Akizungumzia hoja iliyotolewa
na baadhi ya wanasiasa wanaodai kwamba ili uwe rais lazima uwe na uzoefu wa
miaka mingi wa kisasa, alisema zaidi ya marais waliomaliza muda wao na rais
aliyeko madarakani, hakuna Mtanzania mwingine anayeweza kujitapa kuwa na uzoefu
wa kushika nafasi hiyo nyeti ya nchi.
“Uzoefu wa kisiasa wa miaka mingi? Hiyo sio hoja
kwa sababu unaweza kuwa na uzoefu lakini ukashindwa kuyafahamu na kuyafanyia
kazi matatizo ya wananchi,” alisema.
Alisema zaidi ya Rais wa Kwanza wa Tanzania,
Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Tatu, Benjamin
Mkapa na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, hakuna mwingine anayeweza kujisifu
kwamba ana uzoefu huo.
Akitoa mifano alisema kama uzoefu wa kisiasa
kingekuwa kigezo muhimu cha kumpata Rais wa nchi, Mwalimu Julius Nyerere
asingeingia kwenye historia hiyo kwani alichaguliwa kushika nafasi hiyo ya
uongozi akiwa kijana asiye na uzoefu unaozungumzwa.
“Ipo na mifano mingine ya nje ya nchi. Barack
Obama amechaguliwa kuwa Rais wa taifa kubwa kabisa duniani kiuchumi akiwa na
uzoefu wa kisiasa wa miaka mitano tu,” alisema.
Alisema ametangaza nia ya kuwania urais wa nchi
hii baada ya kujiuliza maswali muhimu matatu, mojawapo likiwa ni kama kazi hiyo
ataiweza kwa maana ya kuwa na uwezo wa uongozi, kuwa meneja wa kazi hiyo na
kuhamasisha wananchi kuleta maendeleo. Swali lake la pili, Makamba alisema ni
kama anaweza kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali dini, itikadi wala rangi
zao na la tatu kama ana mawazo mapya yanayoweza kusaidia kuleta mabadiliko ya
kimaendeleo katika nchi.
“Majibu ya maswali hayo yote ni ndio. Nataka
kuona nchi yetu inasonga mbele kwa kasi zaidi. Nina dhamira ya dhati kabisa ya
kuleta aina mpya ya uongozi nchini; swali la nne ninalojiuliza ni kama nitaweza
kushinda, na swali hilo tunaendelea kulifanyia kazi kwa sababu ni lazima ushiriki
kwenye mchezo wenyewe.
Mchakato wa Katiba Aliwataka Watanzania
kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya kuikubali Katiba Inayopendekezwa kwa
sababu ina mambo mengi mapya yatakayowasaidia Watanzania kwa ujumla wao tofauti
na Katiba ya sasa.



0 comments:
Post a Comment