RAIS Jakaya Kikwete amesema atawajibisha
wakurugenzi watakaoshindwa kukamilisha ujenzi wa maabara ifikapo mwezi
ujao kwani katika suala hilo, hatakuwa na mzaha.
Aidha amesema kuanzia
sasa, shule zote za sekondari za Serikali zenye Kidato cha Tano na Sita
zitakuwa za kitaifa, kwa maana ya kuwa na mchanganyiko wa wanafunzi
kutoka maeneo mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kuendeleza utaifa kwa
vijana.
Rais Kikwete ambaye alisema hayo juzi
mjini hapa wakati akifungua kikao kazi cha kujadili usimamizi na
uendeshaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari, aidha amewashukia wakuu wa
mikoa na wilaya akisema ambao hawajui wajibu wao ni bora wasiwepo.
Aliwaambia viongozi hao wa wilaya na
mikoa kwamba, “Kama ajenda yako ni barua na posho ni bora usiwepo.
’’
Wakurugenzi kitanzini Katika kikao hicho kilichoshirikisha wakuu wa
mikoa yote nchini, wakuu wa wilaya, maofisa elimu wa mikoa, Makatibu
Tawala wa Mikoa na maofisa usalama, Kikwete alisema wakurugenzi
wakishindwa kuhakikisha kila shule inakuwa na maabara, kazi itakuwa
imewashinda.
Alisema alishatoa maagizo juu ya ujenzi
wa maabara za sayansi kwani mtoto anayesoma bila maabara, hawezi kufaulu
mtihani wa vitendo.
“Novemba nitauliza sina sababu ya
kusahau, nasubiri Desemba 9, mwaka huu wakati wa miaka 53 ya uhuru
nitauliza maswali na nitadai taarifa hizo lazima nizipate,” alisema.
“Nitamuuliza Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa
Wilaya na Mkurugenzi, kama shule hazina maabara Mkurugenzi kazi
imekushinda nitaanza na wewe, Novemba mwaka huu tutabanana, bado
nitakuwa na mamlaka kamili na sitakuwa na masihara na mtu,” alisema.
Alisema katika ujenzi huo anataka kuwa
na maabara za fizikia, kemia na baolojia. “Kuna mahali nilipita
nikaoneshwa maabara nikanyamaza kimya nasubiri Novemba,” alisema.
Alisema maendeleo yote ya nchi hii yapo mikononi mwa wakurugenzi.
“Lakini kama Mkurugenzi hatimizi wajibu wake kwa nini yupo na kwa nini anaendelea kuwepo?” alihoji.
Shule za utaifa Akifafanua kuhusu utaifa
kwa vijana, alisema kuanzia sasa shule zote za serikali zenye kidato
cha tano na sita zitakuwa za kitaifa na hata zile ambazo ziko kwenye
kata zitabadilishwa na lazima ziwe na mabweni ya kulala wanafunzi.
“ Tunataka kuendeleza utaifa kwa vijana,
tuendelee kuwa na shule za taifa vinginevyo utakuta mtu amezaliwa
Kanyigo amesoma shule ya Msingi Kanyigo, Sekondari Kanyigo, Kidato cha
tano na sita Kanyigo mtu kama huyu anaelewa watu wote duniani ni
Wahaya,” alisema.
Aliendelea kusisitiza, “kidato cha tano
na sita lazima iwe ya taifa mwanafunzi akisoma Bukoba aende Ndanda
(Mtwara) hapo watajua kuchanganyika na vijana kutoka nchi nzima, wasome
shule hizo.”
Pia alisema sasa shule za kata
zinaendelea kutoshelezwa kwa ubora na wanafunzi wengi wanaochaguliwa
kwenda kidato cha tano na sita wanatoka shule za kata.
Kuhusu uhaba wa
walimu, alisema serikali imepunguza tatizo katika shule za msingi na
sekondari ambapo mwaka jana walimu 18,000 waliajiriwa.
Alisema kwenye baadhi ya wilaya, kuna
ziada ya walimu wa sanaa lakini tatizo lililopo ni upungufu wa walimu wa
sayansi na hisabati, tatizo ambalo linaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Mahitaji ni walimu wa sayansi na hisabati 18,277 huku uwezo vyuo vyote
ukiwa ni walimu 2,500.
Aliagiza mwaka 2016 kila mtoto awe na
kitabu chake cha kila somo. Wanafunzi Vyuo Vikuu Pia alisema kumekuwa na
ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu nchini kutoka 40,000
mwaka 2005 hadi kufikia 204,000 na kuweza kufikia Wakenya na kuwapita
Waganda kwa idadi ya wanafunzi
Alisema Serikali imetoa wigo mpana kwa
vyuo vikuu na wanafunzi wote wanapata mikopo na sasa hakuna mwanafunzi
mwenye sifa anayeweza kukosa nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu.
Alisema Chuo Kikuu cha Dodoma
kilichojengwa kwa fedha za ndani, kinachukua wanafunzi 20,000 na lengo
ni kufikia wanafunzi 40,000.
Alisema wanafunzi wataongezeka taratibu
kutokana na chuo hicho kuendelea kujitanua.
Utoro Pia aliwataka viongozi
hao kuhakikisha watoto wanaoandikishwa shule ya msingi wanamaliza
Darasa la Saba tofauti na sasa ambapo wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha
shule. Wakati huo huo, alitaka kulindwa kwa maeneo ya shule yasivamiwe
na wakurugenzi wasaidie vijiji kupata hati.
“Kila shule eneo lake linajulikana lipatiwe hati na liwekewe mipaka ili watu wasiliingilie,” alisema.
Pia alitaka kuwe na matumizi mazuri ya
fedha kwenye masuala ya elimu. Viongozi waoga Alisema viongozi wengi ni
waoga na si wabunifu hasa katika suala la ujenzi wa nyumba za walimu.
Aliwataka wakurugenzi kuacha kugeuza
shule za sekondari yatima kwa kudhani wajibu wao ni kusimamia shule za
msingi tu. “Kila kata ina sekondari kabla ya shule za kata zilikuwa
chini ya wizara lakini sasa shule hizo ni za halmashauri,” alisema.
Alitaka wakurugenzi kusimamia vizuri
walimu wapya waliopo katika maeneo yao wapate mishahara kama
wanavyostahili kwani kucheleweshewa fedha zao ni kutokana na uzembe
unaofanywa na baadhi ya watendaji Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
Hawa Ghasia alisema kikao
hicho cha siku tatu kinahudhuriwa na washiriki 908. Pia alisema kikao
hicho kimeridhia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuwa Chuo Kikuu Huria cha
Taifa.



0 comments:
Post a Comment