MWALIMU wa Shule ya Sekondari ya
Muungano iliyopo mji mdogo wa Himo wilayani Moshi, Richard Ndoile (30),
anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za
kukutwa gesti na mwanafunzi wake wakifanya mapenzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Koka Moita alilieleza gazeti hili jana ofisini kwake, kuwa
tukio la kukamatwa kwa mwalimu huyo lilitokea Oktoba 4, saa 5.00
asubuhi, katika gesti ya Kilimanjaro iliyopo Himo.
Moita alisema mwalimu na mwanafunzi huyo
(jina limehifadhiwa) ambaye anasoma Shule ya Sekondari Muungano Kidato cha
Tatu, walikamatwa baada ya wazazi wa mwanafunzi kumuona binti yao akiwa
amepakiwa kwenye pikipiki ya mwalimu wake, kuelekea mahala
kusikojulikana.
Alisema hatua hiyo iliwafanya kuhamaki na hivyo kuanza kufuatilia mwelekeo wa pikipiki ili kujua hatma ya safari yao hiyo.
Alisema baada ya kuwafuatilia, pikipiki
hiyo ilielekea kwenye gesti hiyo na baada ya kuteremka mtuhumiwa na
binti yao waliingia ndani na kuchukuwa chumba, kwa lengo la kutimiza
haja zao.
Kwa mujibu wa Kamanda Moita, wazazi
waliamua kupiga simu katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Himo kwa lengo
la kutoa taarifa, ambapo polisi walifika lakini hadi mtuhumiwa
anakamatwa tayari walikuwa wameshatekeleza tendo la kujamiiana.
Alisema mwalimu huyo anashikiliwa na
Jeshi la Polisi katika kituo kidogo cha Himo, kwa ajili ya kumfikisha
mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.


0 comments:
Post a Comment