TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza
rasmi kuanza kuboresha Daftari la Wapigakura kuanzia mwezi ujao na kwamba
itakamilisha kazi hiyo Aprili 18 mwakani.
Kwa tangazo hilo la NEC, ni wazi kuwa upigaji
wa kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa, utafanyika siku chache tu baada
ya kukamilika kazi ya uboreshaji wa daftari hilo; na baadaye litatumika kwa
uchaguzi mkuu ujao.
Hata hivyo, tume hiyo imeonesha wasiwasi wa
kukamilisha kazi hiyo kwa wakati, kutokana na serikali kusuasua kutoa fedha za
kufanyia uboreshaji huo, kwani hadi sasa NEC imepatiwa Sh bilioni 15 tu kati ya
Sh bilioni 293 zinazohitajika.
Ucheleweshaji wa kutoa fedha hizo, umekuwa
ukilalamikiwa na tume hiyo kuwa unachelewesha uboreshaji huo, ambao awali
ulikuwa uanze Septemba, lakini umekuwa ukisogezwa mbele kusubiri fedha kutoka
serikalini.
Naibu Katibu Mkuu wa Uandikishaji Wapigakura
wa NEC, Sisti Cariah alisema hata hivyo wana matumaini makubwa ya kupata fedha
zote kwa wakati na kwamba daftari hilo litakamilika ifikapo Aprili 18 na
wanatarajia kuandikisha wapigakura milioni 23.9.
“Uandikishaji huu unafanyika kwa haraka ili
itakapofika wakati wa kupiga kura za maoni (ya Katiba Inayopendekezwa) daftari
liwe limekamilika jambo ambalo tunaamini litakamilika kwa wakati,” alisema.
Juni mwaka huu, NEC ilitangaza kutoa
vitambulisho vipya vya kupiga kura nchini kwa wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya
mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura na ungetekelezwa Septemba
mwaka huu, kwa kugharimu Sh bilioni 293.
Awali, akitoa taarifa ya uboreshaji wa
daftari hilo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye ni Jaji Mkuu mstaafu wa
Zanzibar, Hamid Mohamoud Hamid alisema NEC wanaamini watapokea fedha zaidi
wakati wanaendelea na uboreshaji huo.
Alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura, ungeanza Septemba mwaka huu lakini haikuwezekana, kutokana na
kuchelewa kupatikana kwa fedha kutoka serikalini.
Alisema katika uboreshaji huo, tume imepanga
kufanya majaribio ya uboreshaji wa daftari kwa kutumia mfumo mpya wa ‘Biometric
Voter Registration’ (BVR) katika majimbo matatu ya uchaguzi nchini, ambayo ni
Kawe Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Kilombero katika Halmashauri
ya Mji wa Kilombero na Mlele katika mkoa wa Katavi.
“Kulingana na ratiba ambayo Tume imejipangia,
majaribio ya uboreshaji wa daftari yataanza kufanyika katikati ya Novemba mwaka
huu na tayari Tume imekwishapokea baadhi ya vifaa muhimu vya uandikishaji
ikiwemo Fomu za Uandikishaji na sasa kinachosubiriwa ni kupokea BVR Kits
(vifaa) 250 wakati wowote kuanzia leo,” alisema.
Hamid alisema baada ya majaribio kukamilika,
itafuatiwa na uboreshaji wa jumla katika maeneo mengine kwa wakati mmoja katika
mikoa yote, isipokuwa mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar, ambayo uandikishaji
utafanyika baada ya mikoa mingine kukamilika.
Alisema muda wa uandikishaji ni siku saba
katika kila kituo na uandikishaji umepangwa kufanyika mwanzoni mwa Januari
mwakani hadi katikati ya Februari mwakani katika mikoa yote, isipokuwa Dar es
Salaam na Zanzibar, ambapo uboreshaji utafanyika mwishoni mwa Februari mwakani.
Akizungumzia suala la muda wa kura za maoni,
alisema kwa sasa wanajikita katika uboreshaji wa daftari kutokana na kuwa tume
hiyo, ilishauri serikali kwa sasa daftari la wapigakura kuwa lina kasoro na
ingebidi kuboreshwa, kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ya Katiba pendekezwa.
“Tulishauri kuwa ni vyema kura hiyo ingepigwa
baada ya kukamilika kwa Daftari, hivyo tunategemea kura hiyo ya maoni
itafanyika muda wowote baada ya kukamilika kwa uboreshaji ili haki itendeke,”
alisisitiza.
Mbowe wa Chadema ang’aka
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema NEC haijashirikisha
vyama vya siasa kwenye mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura, jambo
ambalo linatia shaka utekelezaji wake.
Mbowe alisema vyama vya siasa
havijashirikishwa kama wadau kwenye mchakato huo na kwamba taarifa hiyo ya NEC,
ndio wanaisikia kutoka kwa vyombo vya habari na kwamba hawana taarifa rasmi.
“Tume haijatushirikisha na jambo hili ni la
wadau wote na vyama vya siasa ni wadau wakubwa wa suala hili, sasa kama
hatushirikishwi tunasikia tu kutoka kwenu, kwa kweli haya ndio mambo yanayoleta
malumbano,” alisema Mbowe alipohojiwa na gazeti hili jana.
Alisema Tume ya Uchaguzi inavyoonekana
inawasiliana na chama kimoja cha CCM na kuviacha vyama vingine, wakati mchakato
wa uboreshaji Daftari la Wapigakura ni suala la umma, linalopaswa vyama vyote
kushirikishwa.
“Uchaguzi huru na haki unaanzia mapema wakati
wa uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, lakini cha ajabu vyama vya siasa
hatushirikishwi kama wadau kutoa mawazo yetu na kisha ndio Tume itangaze kwa
vyombo vya habari,” alisisitiza Mbowe.
Kuhusu fedha ambazo NEC wamepata hadi sasa ni
Sh bilioni 15, na mahitaji halisi ya uboreshaji daftari hilo ni Sh bilioni 293,
Mbowe alisema fedha zilizopatikana ni chache na haziwezi kutosha kufanya
utekelezaji. Alisema hawajui Tume ina uhakika gani, kama fedha zinazohitajika,
zitapatikana kwa wakati.



0 comments:
Post a Comment