WAKATI mtoto wa mbunge wa Temeke, Sitti Mtemvu akiandamwa na kashfa
ya kughushi umri baada ya kushinda Miss Tanzania 2014, baba mzazi wa
mrembo huyo, Abbas Mtemvu, ameibuka na kudai sakata hilo ni vita ya
kisiasa inayoratibiwa na wapinzani wake ndani ya CCM.
Tangu Sitti atangazwe mshindi Miss Tanzania katika shindano
lililofanyika Oktoba 11 katika ukumbi wa Mlimani City, wadau mbalimbali
wa urembo wamekuwa wakipinga ushindi wake wakidai hakustahili kutokana
na kukosa sifa ikiwamo ya kutokuwa na umri stahiki.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa Vicoba kwenye klabu
ya Jogging ya Temeke A jijini Dar es Salaam, Mtemvu alisema inasikitisha
watu wanaolitaka jimbo hilo kumwandama kwa kashfa binti yake kwa
maslahi yao binafsi ya kisiasa.
Mbunge huyo, alisema kama mtu anataka jimbo hilo aende kwa hoja na
sio kwa majungu na kubainisha kwamba, yeye alichaguliwa na wana- Temeke,
hivyo anayelitaka jimbo hilo aende kwa hoja kwa wananchi na si kupakana
matope.
“Sikilizeni…hili jambo lisifanywe kisiasa, yule binti wanamdhalilisha
sana, inasikitika mtu anaratibu majungu, tena ni matusi makubwa. Sitti
wanamchafua tena wanamwambia kuwa binti niliyemzaa mimi eti mtoto wake,
ambaye ni Tamia Abbas Mtemvu…haya ni matusi, kisa siasa,” alisema Mtemvu
na kuongeza.
Wanapita wanasema Mtemvu kahonga milioni 62 za jimbo, jamani hivi
fedha za mfuko wa jimbo zinatoka kwa namna hiyo, haya yote ni…MNEC
(mjumbe wa NEC), kama utaka jimbo njoo kwa hoja si majungu na
kuchafuana.
“Kwanza kwa taarifa yenu mimi sikuja hapa nikitokea mtaani, nilitoka
kwenye kazi yangu, mimi nilikuwa DC (Mkuu wa Wilaya) tena faili langu
hadi leo linaonyesha niko likizo…embu waambieni hao, kwanza nani
kwaambia watu wa Temeke hatuna hela,” alisema Mtemvu huku akishangiliwa
na baadhi ya wana kikundi hicho.
Licha ya kutomtaja mlengwa lakini wachambuzi wa siasa za Temeke
walisema kuwa kauli hiyo ilielekezwa kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
CCM (NEC), Phares Magesa, ambaye inadaiwa kuwa ameonesha nia ya kugombea
ubunge jimboni humo mwakani.
Magessa, kwa nyakati tofauti amekuwa akishiriki matukio mbalimbali ya
kuimarisha chama hicho Wilaya ya Temeke, huku akitoa misaada mbalimbali
kwa makundi ya kijamii ikiwamo vikundi vya Jogging na wasanii.
Misaada ya hivi karibuni ni pamoja na kuchangia mradi wa maji mtaa wa
Tambukareli na Oktoba 24, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi
wa Jamvi la Katiba.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, Magesa alisema hakuna ukweli
wowote na kwamba hawezi kutumia u-NEC wake kumchafua kiongozi yeyote wa
chama chake.
“Mimi kazi yangu ni kuhakikisha wabunge wangu yeye (Mtemvu) na
Ndugulile wanatekeleza vema ilani ya chama chetu ili ukifika wakati wa
uchaguzi tukainadi kwa wananchi, hivyo siwezi kumhujumu,” alisema.



0 comments:
Post a Comment