SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imetangaza neema kubwa kwa
Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutoa dola za Marekani milioni 85 (Sh
bilioni 140) kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuisaidia Tanzania
kufanya mageuzi ya viwanda.
Neema hiyo ya China kwa Tanzania imetangazwa na Rais Xi Jinping wa
nchi hiyo katika mazungumzo rasmi ya kiserikali kati yake na ujumbe wa
Tanzania, ukiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye yuko katika ziara
rasmi ya siku sita nchini China.
Mazungumzo hayo kwenye Jumba la The Great Hall of the People,
yalifanyika baada ya Rais Kikwete kukaribishwa rasmi katika Jamhuri ya
Watu wa China kwa kupokelewa na Rais Xi Jinping katika eneo la East
Plaza la Jumba hilo.
Katika mapokezi hayo, Rais Kikwete alipigiwa mizinga 21 na kukagua
gwaride la ukakamavu la Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China.
Katika mazungumzo hayo, Rais Xi Jinping alitangaza kuwa China
itaipatia Tanzania kiasi cha dola za Marekani milioni 85 (Sh bilioni
140), ikiwa ni mchanganyiko wa msaada na mkopo usiokuwa na riba, fedha
ambazo Tanzania itaamua yenyewe jinsi gani ya kuzitumia.
“Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania kuboresha
maisha ya wananchi wake, napenda kutangaza kuwa China itatoa kiasi cha
RMB milioni 200 ikiwa ni msaada na RMB milioni 200 nyingine zikiwa ni
mkopo usiokuwa na riba kwa Tanzania.” “… na kiasi cha RMB milioni 100 za
msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zitatumika kwa
kadri Serikali hizo mbili zitakavyoamua,” alisema Rais Jinping.
Rais huyo wa China pia alitangaza kuwa nchi hiyo, itaisaidia Tanzania
katika uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji ya EPZ, uendelezaji wa
miundombinu, itaharakisha ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na itaingia
katika shughuli za kutafuta gesi na mafuta katika ukanda wa Bahari ya
Hindi katika eneo la Tanzania.
Rais Jinping pia alitangaza kuwa Serikali ya China imefanya uamuzi wa
kuikarabati Reli ya TAZARA, inayounganisha Tanzania na Zambia na yenye
urefu wa kilomita 1,860 na kusaidia uendeshaji wa reli hiyo.
“Ili kutekeleza uamuzi huu kwa haraka, napendekeza kuundwa kwa kamati
ya pamoja ya wataalamu kuandaa ramani ya namna ya kuitoa reli hiyo
katika matatizo yake ya sasa,” alisema.
TAZARA ndiyo reli ya kwanza duniani kujengwa na Jamhuri ya Watu wa
China, ambao utaalamu wake sasa unasakwa na nchi nyingine nyingi
duniani.
Rais Jinping pia alitangaza Serikali yake itatoa nafasi 100 za masomo
ya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka Tanzania katika miaka mitano
ijayo, itaongeza idadi ya madaktari ambao China inapeleka Tanzania,
itahimiza kampuni zaidi ya China kuwekeza katika Uchumi wa Tanzania na
kuzishawishi taasisi za kifedha za China kuanzisha shughuli zake katika
Tanzania.



0 comments:
Post a Comment