KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imewafukuza kwenye kikao
timu ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika iliyoongozwa na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo,Sophia Kaduma na kuipa wiki mbili kutekeleza maagizo
kisha kuifuata kamati hiyo mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto, alitoa uamuzi huo jana jijini
Dar es Salaam mara baada ya timu hiyo kujitambulisha mbele ya kamati na
kisha kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo, ambapo majibu yake
hayakuiridhisha kamati.
“Leo tunawarudisha hatukagui mahesabu yenu, jipangeni upya mtufuate
Dodoma baada ya wiki mbili mje na mikakati inayotekelezeka,’’ alisema
Zitto.
Maagizo waliyopewa wizara hiyo wayafanyie kazi na kupeleka majibu
baada ya wiki mbili mjini Dodoma ni kuandaa mkakati unaotekelezeka wa
kununua mazao ya wakulima, ambapo kwa msimu huu wa mavuno, mazao ni
mengi na hakuna masoko.
Agizo la pili wanalotakiwa kulitekeleza na kulipeleka Dodoma ni kuwa
na taarifa inayoonesha jinsi deni la Sh bilioni 3.8 la Kampuni ya Mbolea
ya Minjingu linavyolipwa.
“Mikakati yenu haitoshelezi, haina msaada kwa mkulima ni sawa na
serikali imewaacha wahangaike wenyewe, mahindi ni mengi hakuna soko,
sasa kama hakuna ufumbuzi ni kuwaonea wakulima, ondokeni mkajipange mje
na mkakati wa kununua mahindi ya wakulima kwa msimu huu,’’ alisema
Zitto.
Alisema wamewarudisha wizara hiyo ili wakajipange na kisha waifuate
kamati hiyo mjini Dodoma, baada ya wiki mbili wakiwa na mkakati huo
kwani kuna ziada ya tani milioni mbili za mahindi kwa wakulima ambazo
hazijulikani soko litapatikana wapi.
Awali, Zitto alimtaka Katibu Mkuu huyo kuonesha ni hatua gani wizara
imechukua kuhusu ziada ya mazao yaliyozalishwa na wakulima katika msimu
huu, ambapo mahindi ni mengi na soko hakuna.



0 comments:
Post a Comment