![]() |
| wziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh Mizengo Kayanza Peter Pinda |
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema amevutiwa na kasi
ya mabadiliko katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na hasa
uanzishwaji wa kozi mpya zinazolenga uongezaji thamani wa mazao ya kilimo
(Agri-processing).
Ametoa kauli hiyo wakati
akizungumza na wahadhiri, wakufunzi, wanafunzi na wanajumuiya ya SUA mara baada
ya kutembelea chuo hicho na kukagua utekelezaji wa mradi wa Sayansi na
Teknolojia ya Elimu ya Juu (Science and Technology Higher Education Project –
STHEP).
Amesema kuwa amefurahishwa na suala la Agri-processing kwa sababu hivi tuna mzigo
mkubwa unaoisumbua Serikali nao ni namna ya kununua mazao ya wakulima.
Ameongeza kuwa Tanzania tuna ziada
ya tani milioni 1.5 za mahindi na tani laki nane za mpunga wakati uwezo wa NFRA
ni kununua tani 240,000 tu.
Ameeleza kuwa hayo ni matokeo ya
wahitimu waliotoka SUA na kupelekwa wilayani na vijijini wakahimiza kilimo bora
kwa wananchi.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili
Morogoro akitokea Dodoma, amefanya ziara
ya siku kwa kutembelea Chuo Kikuu hicho pamoja na kiwanda cha kutengeneza nguo
cha 21stCentury.
Akiwa chuoni hapo, Waziri Mkuu
alikagua majengo matatu yaliyojengwa chini ya mradi wa STHEP na kuzindua mawili
kati ya hayo, alitembelea maabara za upimaji ubora wa vyakula na kisha
kuzungumza na wanaSUA.
Akizungumza na wanajumuiya
hao, Waziri Mkuu aliwataka wawe ni viongozi wa mfano kwa kumiliki walau ekari
moja ya shamba, walime au kuweka mifugo ili yale wanayofundisha darasani
yaonekane kwa vitendo katika mashamba hayo.
Mapema,akiwasilisha taarifa
ya mradi wa STHEP, Profesa Gerald Monella alisema mradi huo wenye thamani ya
dola za Marekani milioni 7.48 (sawa na sh. milioni 12.5/-) umekisaidia chuo
hicho kupata majengo manne yenye kati ya ghorofa moja na mbili, ambayo
yameongeza nafasi za kufundishia wanafunzi, vyumba vya maabara na vifaa vyake,
kuanzisha mitaala miwili pamoja na kusomesha walimu 21.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la
Chuo hicho, Mama Kate Kamba wakati akitoa salamu za shukrani kwa Waziri Mkuu,
amesema Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza bajeti ya Chuo kwani kinahitaji
fedha zaidi kwa ajili ya kufanya tafiti na kuboresha miundombinu.



0 comments:
Post a Comment