![]() |
| MAREHEMU Timoth Mroki |
MFANYABIASHARA
wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania Bush Camp yenye kambi za
watalii katika hifadhi za Serengeti mkoani Mara na Manyara iliyopo
katika mikoa ya Arusha na Manyara, Timoth Mroki (36) amejiua kwa
kujipiga risasi tatu kifuani akiwa katika baa maarufu ya Arusha Raha
iliyopo la Shams, jijini hapa.
Kisa
cha kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya kuligonga
gari jingine katika eneo la Mbauda wakati akitokea katika makazi yake
yaliyopo eneo la Kwa Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya baa maarufu ya Arusha Raha.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa hiyo baada
ya kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha bodaboda waliokuwa
wamemzingira katika eneo la ajali na kisha kuondoka kwa kasi kwa gari
lake aina ya Nissan Navara.
“Alipiga
risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguza wakanywea, akatumia mwanya
huo kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha Raha pengine kwa lengo la
kujificha, na hapo akaanza kunywa…
“Ingawa
inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha Raha alikunywa
haraka pombe mbili kali aina ya Valuer na wakati anamalizia ya tatu,
akajikuta anazingirwa tena na wale waendesha bodaboda,” anasema mtoa
habari huyo na kuongeza kuwa, baada ya kufyatua tena risasi mbili
nyingine hewani, lakini bila ya dalili ya watu hao kutishika, ndipo
akaamua kujimiminia risasi.
Habari
zaidi zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi wasamaria
wema wakiwa harakati za kupiga simu polisi walishitukia polisi wakiingia
katika eneo la tukio lakini tayari Mroki alikuwa ameshajitoa uhai baada
ya kujimiminia risasi kifuani.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas hakupatikana kuzungumzia
tukio hilo, ingawa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya Arusha
imekiri kuwepo kwa tukio, lakini chanzo chetu kikikataa kutajwa jina
gazetini kwa kuwa si wasemaji wa matukio ya jeshi hilo mkoani Arusha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.



0 comments:
Post a Comment