![]() |
| Ardhi wilayani Monduli mkoani Arusha,Asema LOWASA |
WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa
amesema kuwa tatizo la ardhi wilayani Monduli mkoani Arusha ni kubwa
kuliko inavyofikiriwa na umasikini unapiga hodi kwa kasi kubwa katika
wilaya hiyo, kutokana na uuzwaji holela wa ardhi kwa thamani ndogo.
Lowassa alisema hayo jana katika semina
ya siku mbili ya kutatua tatizo la migogoro ya ardhi iliyokithiri katika
wilaya hiyo, semina iliyohusisha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Serikali ngazi ya wilaya, kata, kijiji na tawi na viongozi wa mila ya
jamii ya Kimasai wanaojulikana kwa jina la Laigwanani.
Alisema watu wanaongezeka katika wilaya
ya Monduli lakini ardhi kamwe haiwezi kuongezeka lakini Laigwanani kwa
kushirikiana na viongozi wa vijiji wanakula rushwa na kuuza ardhi kwa
bei ndogo kwa maslahi yao, kitu ambacho ni hatari kubwa kwa wakazi wa
Monduli.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Monduli na pia alikuwa Mwenyekiti wa semina hiyo, alisema hivi sasa
wajane wengi wamekuwa wakidhulumiwa na viongozi wa mila na vijiji kwa
kunyang’anywa ardhi na kuwafanya kuhangaika huku na kule bila ya sababu
za msingi, na aliwataka viongozi kuacha kufanya hivyo mara moja kwani
hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema kibaya zaidi Laigwanani na
viongozi wa vijiji wanauza ardhi kwa rushwa kidogo ama kwa kununuliwa
kinywaji na kutoa ardhi yenye thamani kubwa kwa bei ndogo, hiyo ni
hatari kwa vizazi vijavyo.
Lowassa alisema kuuza ardhi ni sawa na
kuuza utajiri na kununua umasikini na kusema kuwa itafika wakati
wananchi wa Monduli watakuwa masikini wa kupindukia kwa kufanya maamuzi
hayo yasiyokuwa na maana jamii ijayo.
Lowassa alisema enzi za Waziri Mkuu
Edward Sokoine, vijiji viliamriwa kutoa ardhi kwa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya shughuli zao za mafunzo na
wafugaji walikuwa wakilisha mifugo yao bila ya shida, lakini kwa sasa
kuna wajanja wachache wanataka fidia kwa kitu ambacho hakipo hiyo
haitawezekana kamwe.



0 comments:
Post a Comment